MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Sibwesa katika Wilaya ya Tanganyika, Peter Ngomalala (50) kifungo cha maisha baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa, mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi wilayani Tanganyika huku mtoto mwenzake wa kike mwenye umri wa miaka saba akishuhudia.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Chiganga Ntengwa alisoma hukumu hiyo jana alisema ameridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Flavian Shiyo uliwaita mashahidi kadhaa akiwemo mtoto huyo aliyebakwa na pia mama yake mzazi. Hakimu alisema mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha Sheria namba 130 (1)(2) na kifungu cha Sheria 131 (3) kanuni ya adhabu.
Alisema mtoto mwingine aliyeshuhudia na aliyebakwa wote pamoja na kuwa na umri mdogo, bado walitoa ushahidi kwa ufasaha ambao haukuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Hakimu alisema mahakama hiyo ilijiridhisha na ushahidi wa muuguzi wa zahanati ya Sibwesa mtoto huyo alikofanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kupewa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs).
Awali Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Shiyo alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 12, 2016 saa 4 asubuhi kijijini Sibwesa ambapo alimkuta mtoto huyo akicheza na mwenzake jirani na kwao akawalaghai watoto hao wamfuate nyumbani kwake akawape fedha wanunue biskuti na vinywaji baridi.
Wakili Shiyo alidai kabla hajafika nyumbani kwake alimvuta mtoto huyo kwa nguvu na kumpeleka eneo la tangi la maji na kumbaka huku mwenzake akishuhudia tukio hilo na licha ya watoto hao kupiga kelele za kuomba msaada hakumwachia.
Ilidaiwa watoto hao waliwataarifu wazazi wao ambako mshtakiwa alitiwa nguvuni na askari mgambo wa kijijini humo na kumfikisha katika kituo cha polisi. Mshitakiwa alijitetea akidai hakumfanyia mtoto huyo unyama huo, bali mama yake mzazi amemsingizia kwa kuwa alikuwa akimdai fedha alizomkopesha hivyo kuomba mahakama imwachie huru
0 Comments