TAARIFA kuwa hakuna mtu aliyehusika kusababisha mimba kwa wanafunzi 325 aliyefungwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, zimemshitua Mkuu mpya wa Mkoa (RC) wa Rukwa, Joachim Wangabo; imefahamika.
Kutokana na hali hiyo, Wangabo alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa, George Kyando kufuatilia na kujua kama kuna kesi zozote za wanafunzi kupewa mimba katika vituo vya polisi, ili ahakikishe zinafikishwa mahakamani haraka.
Aliwataka wakuu wa wilaya wakiwa ni wenyeviti wa kamati za maadili katika wilaya zao, kuitisha vikao vya maadili na mahakimu ili wajadili mienendo ya utendaji wa mahakimu hao na kama wapo “waliochezea” kesi hizo, basi wachukuliwe hatua stahiki kwa kwenda kinyume na maadili ya kazi. Alitoa maagizo hayo jana wakati wa makabidhiano ya madaraka na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Zelothe Steven katika hafla iliyohudhuriwa na wakuu wote wa wilaya.
Kwa upande wake, Zelothe aliyestaafu utumishi wa umma aliwataka watumishi wa umma, viongozi wa dini, mila na wananchi wote wampe ushirikiano mkuu huyo mpya wa mkoa. Alisema tatizo la mimba shuleni katika mkoa huo ni changamoto kubwa, kwani limesababisha wanafunzi 325 kukatiza masomo. Kati yao, 288 walikuwa wakisoma katika shule za sekondari na 37 wakiwa wa shule za msingi.
Alisema Wilaya ya Nkasi inaongoza kimkoa kwa kuwa na wanafunzi 152 waliopewa ujauzito katika kipindi hicho. “Yapo malalamiko mengi wananchi wanalalamika hakuna hukumu yoyote iliyotolewa mahakamani kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili kwa kesi zote 325 za wanafunzi waliokatiza masomo yao baada ya kupewa ujauzito licha ya kesi hizo kuripotiwa katika vituo vya polisi ... Zipo pia taarifa za kesi hizo kuchezewa mahakamani yaani hakuna mhusika yeyote aliyewapatia mimba wanafunzi hao aliyefungwa katika kipindi chote hicho. Hii haikubaliki,” alisisitiza Wangabo.
“Lazima hatua za kisheria zichukuliwe kesi hizo zote lazima zishughulikiwe haraka iwezekanavyo na nikifanya ziara katika wilaya zenu nipewe taarifa hizi. Hili siwezi kulifumbia macho.” Sheria inasema mwanamume anayesababisha ujauzito kwa mwanafunzi, mzazi au mlezi anayetoa taarifa za uongo kuhusu ujauzito aliopata mwanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwaozesha na wanaowafungisha ndoa wanafunzi, wakibainika adhabu yao ni kifungo cha miaka 30 jela.
0 Comments