TUMEJIPANGA VEMA KUBORESHA ELIMU YETU - PROF NDALICHAKO

IN SUMMARY

Ameeleza namna Serikali ilivyoweka mipango ya uboreshaji miundombinu ya kufundishia.

Paris. Serikali imesema itahakikisha inafikia malengo ya maendeleo endelevu yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu bure, uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, vyuo vya ualimu na kuboresha mazingira kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati akihutubia mkutano mkuu wa 39 wa Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) unaoendelea Paris, Ufaransa.

Amesema ili kufikia malengo hayo walimu 68,799 wamepatiwa mafunzo maalumu ya mtalaa ulioboreshwa wa Kusoma, Kuhesabu na Kuandika (KKK).

Waziri Ndalichako alisema suala la wanafunzi wenye mahitaji maalumu bado linahitaji kuangaliwa kwa mapana zaidi na kuziomba nchi wanachama kutoa kipaumbele katika kuandaa mazingira ambayo yatakuwa rafiki kwa wanafunzi wa kike na wa kiume wenye mahitaji maalumu.

Pia, Waziri Ndalichako amesema Serikali imekwisha anza kutoa elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne.

Amesema tayari vifaa vya maabara na vitabu kwa shule za Sekondari vimesambazwa kwa nchi nzima ili kutilia mkazo masomo ya sayansi. 

Waziri Ndalichako pia ameshiriki mikutano mbalimbali inayohusu tume za Unesco zilizoanza Oktoba 30, 2017 ambapo amepokea taarifa zinazohusu fursa mbalimbali za namna ya kupata misaada ya maendeleo kutoka Unesco na washirika wake wa kimataifa.

Pia, kupitia mkutano huo Mkuu viongozi wa Tume za Taifa za Unesco duniani wanapata fursa ya kukutana na kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mbalimbali za kuandika kazi miradi kwa maslahi ya nchi zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Unesco, Irina Bokova amesema kumekuwa na mafanikio makubwa yanayopatikana kutokana na ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama na kuwaomba kuuendeleza zaidi.

   

 

0 Comments