MWALIMU MKUU AMCHARAZA VIBOKO MWALIMU MWENZAKE


Kwa ufupi

Lugumba alisema baada ya kupata taarifa za mwalimu huyo kuchapwa viboko Ijumaa iliyopita, uongozi wa CWT ulifika Runazi kujiridhisha ambako wanafunzi na wazazi walithibitisha tukio hilo ikidaiwa kwamba mwalimu huyo alifungwa kamba kwenye mti.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Migango wilayani hapa amemchapa viboko mwalimu mwenzake mbele ya wanafunzi akimtuhumu kwa wizi wa sahani tano pamoja na nusu kilo ya sukari iliyotolewa kwa ajili ya mahafali ya wahitimu wa darasa la saba.

Katika taarifa yake ya kulaani kitendo hicho, kaimu katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Biharamulo, Joseph Lugumba alisema mwalimu mkuu, Mateso Musaku alimpiga viboko mwalimu wake Hosea Masatu mbele ya wanafunzi tukio ambalo linalaaniwa na wazazi, uongozi wa CWT na jamii ya Kata ya Runazi wanakoishi walimu wa shule hiyo.

Lugumba alisema baada ya kupata taarifa za mwalimu huyo kuchapwa viboko Ijumaa iliyopita, uongozi wa CWT ulifika Runazi kujiridhisha ambako wanafunzi na wazazi walithibitisha tukio hilo ikidaiwa kwamba mwalimu huyo alifungwa kamba kwenye mti.

Alisema mwalimu Masatu alidaiwa kuiba vitu hivyo siku moja baada ya kumalizika mahafali ya darasa la saba na kwamba alipoulizwa alikiri.

Alisema mbali ya kuonywa, alipelekwa na kufungwa kamba chini ya mti na kuchapwa mbele ya wanafunzi kitendo alichokiita cha udhalilishaji na kinyume cha haki za mtumishi na binadamu.

“Tunashauri mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kwa kutumia mamlaka zilizomteua mwalimu mkuu huyo kuongoza shule hiyo amuwajibishe kwenye ngazi za kinidhamu kwa maana amekiuka kanuni za uteuzi katika kuongoza walio chini yake,” alisema Lugunda.

Imeelezwa kuwa tukio hilo lilitokea Novemba Mosi baada ya mwalimu Masatu kukamatwa saa nane mchana na mkuu wa shule na kufungwa katika mti uliopo mbele ya shule hiyo na kuchapwa viboko saba huku wanafunzi wakishuhudia.

Mwalimu Musaku alithibitisha kumchapa mwenzake kwa madai kwamba alipata ridhaa kutoka kwa mwalimu aliyetuhumiwa kwa wizi na hakufikiria kama suala hilo lingeweza kuleta matokeo hasi katika jamii.

Alisema kwamba katika madaraka aliyopewa hakuna kipengele kinachomruhusu kutoa adhabu kama hiyo ya kipigo na kwamba ilitumika baada ya mwalimu huyo kukiri kosa na kutaka apewe adhabu ya viboko saba.

Hata hivyo, mwalimu Masatu alisema kitendo cha kupigwa na mkuu wake wa kazi kwa tuhuma za wizi wa mali ya shule ni udhalilishaji.

Alisema baada ya tukio la kupigwa alipelekwa kituo kidogo cha Polisi Runazi ambako alikaa rumande kwa siku tatu kwa madai ya kulewa saa za kazi na aliachiwa Novemba 3.

Hata hivyo, Polisi wilayani Biharamulo hawakutaka kuzungumzia suala hilo.

Kutokana na tukio hilo, Mwalimu Masatu alisema hana amani katika kata ya Runazi na Wilaya ya Biharamulo kutokana na taarifa za tukio hilo la kudhalilishwa kwake kusambaa.

Alisema hana imani kama ataingia darasani na kufundisha ipasavyo kwani ameathirika kisaikolojia. Aidha, alikana madai ya kuiba sukari na sahani tano na kwamba ametuma malalamiko kwa mratibu elimu kata na mwenyekiti wa kamati ya shule ili wachukue hatua dhidi ya mkuu wake kumdhalilisha kiutumishi na kijamii.

Walimu katika Shule ya Msingi Migango, Francisco Leonard na Faustine Mathias walioshuhudia tukio hilo walisema kitendo alichofanyiwa mwenzao ni udhalilishaji na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuanzia kamati ya shule hiyo mpaka ofisi ya mkuu wa wilaya zifuatilie na kujiridhisha juu ya ushahidi utakaotolewa ili kuhakikisha mwalimu aliyedhalilishwa anatendewa haki kwani kila anakopita ananyooshewa vidole na kukosa amani kuanzia kwenye familia yake.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Wende Ng’ahala alisema japokuwa hajapewa taarifa anajipanga kulishughulikia.

   

 

0 Comments