WALIMU WATUHUMIWA 'KUOA' WANAFUNZI WAO- MPANDA

BAADHI ya walimu wanaofundisha katika Shule za Sekondari za Katumba na Nkeswa zilizopo katika kambi ya wakimbizi ya Katumba wilayani Mpanda katika mkoa wa Katavi, wanatuhumiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao wa kike.

Aidha imeelezwa kuwa mmoja wao “amemuoa” mwanafunzi wake kwa kumtolea mahari kwa wazazi wake. Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , George Kakunda alielezwa hayo na Diwani wa Kata ya Katumba iliyopo katika Halmashauri ya Nsimbo, Seneta Baraka wakati alipokutana na madiwani na watumishi wa halmashauri ya Nsimbo katika majumuisho ya ziara yake ya siku moja aliyoifanya mkoani Katavi.

Akimsimulia mikasa ya walimu hao, Diwani Baraka alisema: “Nilishatoa taarifa ya mwalimu aliyemweka kinyumba mwanafunzi wake wa kike pia walimu wenye mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao wa kike katika vikao vya baraza la madiwani, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yao badala yake baadhi ya madiwani wenzangu wamevujisha siri za vikao na kwenda kuwataarifu walimu hao kuwa mimi ndio ninayewashtaki,” alieleza

0 Comments