Viongozi wanafunzi elimu ya juu walia mikopo ‘kiduchu’
Kwa ufupi
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya viongozi wa wanafunzi walisema bajeti hiyo imekuwa ikizidi kupungua licha ya wanafunzi kuongezeka.
Siku moja baada ya Serikali kusema imeidhinisha Sh427 bilioni za mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/18, viongozi wa wanafunzi wamelalamikia bajeti hiyo kuwa ni ndogo ukilinganisha na mahitaji.
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya viongozi wa wanafunzi walisema bajeti hiyo imekuwa ikizidi kupungua licha ya wanafunzi kuongezeka.
Mkurugenzi wa haki za wanafunzi wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo alisema mwaka 2016/17 Serikali ilitenga Sh483 bilioni kwa wanafunzi 120,000 ikiwa ni ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu itakayowasaidia kujikimu pindi wanapokuwa vyuoni.
“Cha kushangaza mwaka wa masomo 2017/18 wanafunzi wameongezeka na kufikia 122,000, lakini badala ya fedha za mkopo kuongezeka zimepungua na kuwa Sh427 bilioni waombaji wakiwa 61,000 na Serikali imesema itawapa 30,000 pekee,” alisema.
Akilifafanua hilo, naibu waziri wa Elimu, William Ole Nasha alisema Serikali imetenga fedha hizo kulingana na maombi ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB). Alisema kwa kuzingatia hilo ndiyo maana tayari Sh147 bilioni za robo ya kwanza ya mwaka wa masomo 2017/18 zimeshaingizwa kwenye akaunti ya HESLB na itatakiwa hadi mwisho wa wiki hii ziwe zimeshasambazwa vyuoni.
“Kuna vigezo ambavyo vimewekwa na kulingana na vigezo hivyo bodi imejiridhisha fedha hizo zinatosha, bodi ingeomba halafu Serikali ingepunguza lawama hizo zingekuwa na tija,” alisema Ole Nasha.
Kwa upande wa waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi wa UDSM, Juma Matata alisema miaka ya nyuma fedha zilikuwa hakuna, lakini mwaka jana bodi imekusanya fedha nyingi za madeni, lakini bado bajeti imekuwa finyu.
Alisema vigezo vinavyotumika ni ngumu kubaini ukweli wake kwa sababu si kila anayeishi katika familia bora ana uwezo akisema, “Wengine wanalelewa tu kwa jamaa zao na wazazi wao hawana uwezo wa kumudu gharama za vyuoni,”
Mkurugenzi wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema changamoto iliyopo ni baadhi ya wanafunzi na wazazi kuamini hata kama wana uwezo ni lazima wapate mkopo.
“Siyo kweli kwamba wanafunzi Tanzania nzima hawana uwezo wa kumudu gharama za kusoma vyuoni, ila imejengeka dhana kuwa wakifika chuo kikuu lazima walipiwe na Serikali,” alisema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Stanslaus Kadugalize aliwataka wanafunzi wote walioomba mikopo watulie hadi bodi imalize kazi yake ya kupanga kulingana na sifa zao na hapo watajua wafanye nini kuwasaidia watakaokosa.
0 Comments