WIZARA IDHIBITI WANAFUNZI KUTOMALIZA SHULE

Uboreshaji huo umo katika Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem) mwaka 2001 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (Mmes) wa mwaka 2006.

Uboreshaji elimu uliyoanza mwanzoni mwa milenia ulilenga kuhakikisha kuwa kila mtoto aliyefikia umri wa kuanza shule, anafata nafasi hiyo na baadaye kila mwanafunzi anayefanya vizuri anapanga ngazi.

Uboreshaji huo umo katika Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem) mwaka 2001 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (Mmes) wa mwaka 2006.

Kupitia Mmem, shule mpya za msingi zilijengwa, madarasa yaliongezwa katika shule za zamani na nyingine ziligawanywa kuwa na shule mbili tofauti, yaani Shule “A” na “B” au zilizopewa majina tofauti. Taarifa za Serikali zimekuwa zikionyesha idadi kubwa ya watoto wanaoandikishwa elimu ya msingi.

Ili kuhakikisha idadi hiyo haihangaiki, Mmes iliongeza majengo ya sekondari, walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na vitabu. Mpango huu ndio ulihakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari na hivyo shule hizo kujulikana kama shule za kata.

Japokuwa mwanzoni zilidharauliwa, shule hizo zimechangia sana katika ongezeko siyo tu la wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza, bali hata la wanaohitimu.

Mfano kufikia mwaka 2016 kulikuwa na jumla ya watahiniwa 408,372 wa shule za sekondari na mwaka huu ilitarajiwa idadi ingekuwa kubwa zaidi. Lakini imekuwa tofauti, kwamba katika kipindi ambacho shule ni nyingi, vivutio vimeongezeka na kiu ya kutaka kusoma ni kubwa idadi yao imepungua hadi kufikia 385,938.

Katika taarifa yake, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limesema watahiniwa 385,938 ndio walitarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne kuanzia jana hadi Novemba 17, idadi hiyo ni pungufu ya watahiniwa 22,434 ikilinganishwa na mwaka 2016. Hapo ndipo tunahoji kulikoni?

Mwaka 2016 kulikuwa na jumla ya watahiniwa 408,372 na kati yao watahiniwa wa shule walikuwa 355,822 na wa kujitegemea 52,550. Mwaka huu, watahiniwa wa shule ni 323,513 ambao ni pungufu ya watahiniwa 32,309 ikilinganishwa na mwaka 2016.

Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, mwaka huu wapo 62,425 ikiwa ni ongezeko la watahiniwa 9,875 ikilinganishwa na mwaka 2016 walipokuwa 52,550.

Baadhi ya sababu za kihistoria zinazotajwa kuwa zinachangia upungufu ni utoro, wasichana kupata mimba, familia kukosa mwamko na umaskini. Ikiwa sababu hizo ni za kweli, tunashauri serikali itumie uwezo wake na ushawishi kuzuia hali hiyo.

Kwa upande wa mimba tunashauri sheria zinazomlinda mtoto wa kike na hasa Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 ambayo ni mahususi kushughulikia wanaowapa ujauzito wanafunzi, zitumike kikamilifu.

Mamlaka husika zisifurahie kuorodhesha sababu za kushuka kwa idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kuhitimu, bali zikijikite kuzidhibiti maana katika zama hizi ambazo Serikali imeweka mikakati ya uchumi wa viwanda, pia watahitajika wasomi ambao itakuwa nguvu kazi muhimu.

Aidha tunapongeza juhudi za kuendelea kuongeza idadi ya wasichana. Mfano mwaka huu kati ya watahiniwa 323,513 wa shule waliosajiliwa, wavulana ni 159,103 sawa na asilimia 49.18 na wasichana ni 164,410 sawa na asilimia 50.82.

Kwa hiyo mimba zikidhibitiwa katika ngazi zote katika shule za msingi na sekondari, huenda idadi yao ikawa kubwa zaidi.

Tunawatakia wanafunzi wote kila la kheri katika mitihani yao.

   

 

0 Comments