BODI YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU YATANGAZA MFUMO MPYA.


BODI ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeanzisha utaratibu mpya ambao unamuwezesha mwanafunzi wa chuo kupata mkopo wake ndani ya muda mfupi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Mawasiliano wa Bodi hiyo, Omega Ngole alisema Bodi imeamua kubadili utaratibu uliokuwa ukitumika awali kuwalipa wanafunzi ‘boom’ zao baada ya kuonesha kuwa utaratibu ule wa zamani ulikuwa na changamoto mbalimbali.

“Bodi tumeboresha mfumo, utaratibu wa kuwalipa wanafunzi na kuachana na ule ambao tulikuwa tukitumia awali, sasa hivi mwanafunzi akishatoa akaunti yake ndani ya muda mchache anakuwa ameshaingiziwa fedha zake kwenye akaunti yake,” alisema.

Alifafanua mfumo wa sasa ambao ni wa kielekroniki alisema mfumo huo ni bora kwani Bodi inakuwa na uhakika kwamba fedha zimepokelewa na mwanafunzi husika moja kwa moja, ndani ya muda mfupi na pia inaondoa usumbufu wa matumizi ya makaratasi ambao ulikuwa ukitumika.

Kwa utaratibu huu mpya ambao umesambazwa katika vyuo vyote, unawataka wanafunzi kuingia katika mfumo wa CLAS:https//olas. heslb.go.tz, kujaza fomu na index namba, kujaza akaunti inayopokelea fedha, kuweka namba ya siri na kuweka picha.

Utaratibu huo ni wa siku saba yaani kuanzia Januari 22 hadi 28 mwaka huu. “Utaratibu huu ni kwa wanafunzi wa mwaka wa pili na wale ambao wanaendelea na masomo ambao wakati wanajisajili mfumo ulikuwa haumtaki kuweka picha, kwa hiyo ndiyo tunaowataka kuboresha taarifa zao,” alisema.

Ngole alisema wanafunzi wa mwaka wa kwanza walipokuwa wanajisajili walikuta tayari mfumo huo mpya upo, hivyo waliweka picha zao. Aidha, alisema changamoto kubwa katika mfumo au utaratibu waliouacha ilikuwa baada ya Bodi kupewa majina ya wanafunzi wanaostahili kupewa mkopo pamoja na vyuo walivyopo, Bodi ilituma fedha kwenye vyuo na makaratasi kutumwa kwenye vyuo ili wanafunzi wasaini na kisha makaratasi hayo kurudishwa Bodi.

“Sasa hii ilikuwa ni changamoto, karatasi zinaweza kuchukua hata wiki mbili na wakati mwingine karatasi zimeshafika vyuoni karatasi ina orodha za wanafunzi 200 mpaka wote wapatikane kusaini ndipo irudi Bodi... muda unapotea,” alisema Ngole na kuongeza kuwa utaratibu wa sasa unafupisha mzunguko huo.

0 Comments