JESHI LA POLISI LAKAGUA MAGARI YANAYOBEBA WANAFUNZI - ARUSHA.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Chuo Cha Ufundi Arusha wamefanya ukaguzi kwenye Magari yote yanayobeba wanafunzi, hii leo wamekagua magari ya Jiji la Arusha.

Ukaguzi huu umefanywa ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kikao kati ya Jeshi la Polisi na Wamiliki wa Shule binafsi, wamiliki wa magari ya kusafirisha wanafunzi, Ukaguzi huu umeongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ndugu Charles Mkumbo akiwa Chuo cha Ufundi Arusha.

Kamanda Mkumbo alisema leo imekua ni siku maalum ya ukaguzi kwa magari haya yanayotumika kubeba wanafunzi ili kujua kama magari hayo yamekidhi ubora wa kubeba wanafunzi badala ya kungoja mpaka ajali ikitokea ndio tuanze kukimbia kimbia.

Kamanda Mkumbo ameeleza zaidi kuwa magari yatayogundulika kuwa na hitilafu watayatoa namba za usajili mpaka wamiliki watakapoyarekebisha na kukidhi vigezo ndipo watarejeshewa namba za usajili kisha waendelee kutoa huduma ya usafiri kwa wanafunzi.

Kamanda Mkumbo pia amesema wameufanya ukaguzi huu siku ya Jumamosi ili wamiliki wote wapate nafasi ya kushiriki, na kwa leo yalijitokeza magari sitini (60) na magari ishirini na manne (24) yameonekana kuwa na itilafu hivyo Jeshi la Polisi limelazimika kung'oa namba za usajili ili kuwapa nafasi wamiliki kwenda kuyarekebisha.

Hatahivyo Kamanda Mkumbo amedai kwamba wameamua kufanya ukaguzi huo kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha kwa kuwa ni Chuo bora na chenye vifaa vya kisasa vya ufundi na ukaguzi wa magari.

Wakati akihitimisha mazungumzo yake Kamanda Mkumbo amewashauri wamiliki wa magari wanaotoa huduma ya usafiri kufanya ukaguzi wa magari yao kila mara na wamiliki wengine wa magari yakusafirisha wanafunzi ambao leo hawakupeleka magari yao kwenye ukaguzi wayaleke Chuo cha Ufundi Arusha kwa ajili ya ukaguzi wasisubiri wapigwe faini.

0 Comments