Ibrahim Yamola
Kwa ufupi
Nikiangalia matatizo yanayoikabili sekta ya elimu nchini katika dhana hii ya elimu bure au elimu bila malipo, napata shaka je safari ya kuandaa kizazi imara na chenye kuhoji kitapatikana?
Ni elimu bure au elimu bila malipo? Hapa kumekuwa na uelewa wa nini maana ya kile kinachomaanishwa na Serikali, katika kutekeleza sera ya kutoa elimu kwani kila mmoja amekuwa na uelewa anaoujua yeye.
Nikiangalia matatizo yanayoikabili sekta ya elimu nchini katika dhana hii ya elimu bure au elimu bila malipo, napata shaka je safari ya kuandaa kizazi imara na chenye kuhoji kitapatikana?
Hivi tunatambua ukweli kwamba ubora wa taifa lolote lile hutegemea na ubora wa elimu itolewayo kwa watu wake. Ukikosea kumwelekeza mtu njia hata kufika aendako ni tatizo, vivyo hivyo katika elimu tunayoitoa.
Aprili 18, mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2017/18 alitoa ufafanuzi wa suala hilo.
Simbachawene alisema: “Kuna tofauti kati ya elimumsingi bure na elimumsingi bila malipo. Serikali inatoa elimu elimumsingi bila malipo si elimumsingi bure.”
“Wananchi wanakuwa wazito kujitolea hata nguvu zao katika kuchangia shughuli mbalimbali zinazohusu elimu kwa kisingizio kuwa Serikali ya awamu ya tano inatoa elimumsingi bure,” alisema Simbachawene.
Waziri huyo aliongeza: “Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba waheshimiwa wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wa mamlaka za Serikali, asasi zisizo za kiserikali na wadau wengine wa elimu.
“Wazazi na walezi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha uwepo wa miundombinu muhimu ya shule kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali, msingi na sekondari.”
Maneno haya na kilichopo sasa kwenye jamii, vinanisukuma kuuliza, kwa nini kuwe na sintofahamu isiyo na mwisho? Hivi kama nchi tunashindwa nini kutoa elimu bure isiyo na michango ya aina yoyote?
Tayari kumekuwa na mvutano katika baadhi ya halmashauri kwa madiwani wake kugawanyika. Wapo wanaosema wachangie na wapo wanaodai Serikali ibebe jukumu lote la kutoa elimu bure.
Naungana na kauli aliyoitoa Rais John Magufuli siku alipokutana na mawaziri wake wawili ambao wizara zao zinahusika na sekta ya elimu.
Hawa ni Profesa Joyce Ndalichako na Suleiman Jafo. Alipiga marufuku michango na kama ikibidi, kamati za shule zihusike na walimu wasishiriki.
Hata hivyo, najiuliza kama Taifa, hatuwezi kugharimia elimu bure na ikawa bure kwelikweli? Naamini Serikali inaweza kumhudumia mtoto anapoanza darasa la awali hadi kidato cha nne.
Ugumu upo wapi, kitu gani ambacho hatuna? Mbona tuna rasilimali lukuki zinazoweza kutuingizia fedha na tukazielekeza katika elimu bora na si bora elimu?
Ikumbukwe kuwa utawala wa awamu ya tano tangu ulipoingia madarakani Novemba 5, 2015, ulitangaza kupunguza matumizi ya Serikali kama vile kuzuia safari za nje ya nchi na semina zisizo na tija, kuondoa watumishi hewa na hata kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Kwa muda mfupi, wananchi tukawa tunapewa taarifa za makusanyo makubwa ya mapato kutoka vyanzo mbalimbali. Huu ni ushahidi kumbe nchi ina fedha nyingi kama itaamua kukusanya kama inavyofanya Serikali ya sasa.
Kama yote hayo yamewezekana, ugumu unakuwa wapi kutoa elimu bure isiyohitaji mzazi kuchangia chochote? Kuondoa ada lakini bado mzazi achangie gharama nyingine bado ni mzigo kwa wazazi wengi.
Kwa rasilimali zilizopo na kwa ukweli kwa uongozi huu umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzuia mianya ya matumizi mabaya ya fedha za umma, Serikali inaweza kabisa kufadhili kila kitu, hali itakayotuondolea kero hii ya sintofahamu ya wazazi wachangie au la.
Tunapaswa kuwekeza katika elimu bila ya kuleta masihara. Elimu yetu inapaswa kumwandaa mwanafunzi kwenda kujiajiri na hili lianzie kwa walimu wao wanaotakiwa kuandaliwa kwa kiwango cha kutosha.
Tunaweza kujikita katika eneo la uandikishaji wa wanafunzi na kutoa elimu tukasahau eneo nyeti la walimu, mahitaji yao hasa maeneo ya makazi na maandalizi yao ya jinsi wanavyopatikana.
Kwa mfano, tujiulize, walimu wetu wana fursa ya mafunzo kazini? Kama hayapo tunajipangaje kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia? Haiwezekani mwalimu akakaa miaka miwili au mitatu hajapata mafunzo ya kumweka sawa kimaarifa na kwa mbinu za ufundishaji. Huku ni kujidanganya.
Wahenga walisema elimu bora ni ufunguo wa maisha (bora). Ikiwa hivi ndivyo, basi elimu mbaya itakuwa ni ufunguo wa maisha mabaya. Lakini kila mmoja ajiulize je, elimu itolewayo kwa sasa ni ufunguo wa maisha bora au ni ufunguo wa matatizo?
Vijana wanasoma kwa malengo au wanasoma wahitimu na hatimaye wapate kazi? Tubadilike kwa kuwa tunahitaji kuwa Taifa shindani si tu kwa Afrika Mashariki bali duniani kote.
0716386168
0 Comments