HONGERA SANA JOHN MSHINDI WA PILI MAHAKAMA KUU, UINGEREZA.


Ndugu zangu,

Kijana wetu John jana alimwongoza mwenzake kwenye Mock Court pale Supreme Court ( Mahakama Kuu) kupambana na wenzao wawili mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Uingereza.

John ameniambia wamepambana lakini wapinzani wao waliwashinda kiufundi. Kwa maneno yake mwenyewe anasema kwake kufika fainali na kushika nafasi ya pili ni ushindi mkubwa pia; ni ile hali ya kusimama mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu na kujenga hoja za utetezi. Amesema tukio la jana limemjenga zaidi kwenye kujiamini.

Kama wazazi tunajivunia mafanikio yake. John kama ilivyo kwa nduguze, haamini katika kushindwa bila kupambana . Hakati wala hauna wa kumkatisha tamaa anapoamua kufanya jambo. John anajiamini.

Nakumbuka akiwa mtoto ( Picha ya kati) nilikuwa kocha wa timu ya watoto kule Sweden ambapo kaka yake Olle ndiye alikuwa na umri sahihi wa kuwa kwenye timu hiyo. Lakini, John akaniambia naye anataka kucheza timu hiyo. Sasa kazi kwenye jezi, ni kubwa, lakini akaivaa hivyo hivyo huku ikimfika miguuni!

Alipojua kuwa timu kwenye mechi ina captain, siku moja tukienda kwenye mechi akaniambia;
" Baba leo mimi nataka niwe captain wa timu."
Nilipomwambia kuwa captain lazima acheze kutoka mwanzo wakati yeye John nimepanga kumwingiza kipindi cha pili, akanijibu;

" Basi, nipange kucheza tangu mwanzo na niwe captain!"

Si ajabu, kwenye Chuo Kikuu anachosoma, akiwa mwaka wa kwanza amegombea kuwa Kiongozi wa Wanafunzi wa mwaka wa kwanza na amechaguliwa. Na juzi hapa amewaongoza wenzake wanne kwenye shindano la Laywers Without Borders kwenye mada ya Wildlife Trafficking na wakaibuka washindi wa kwanza.

Hongera Sana John!!

0 Comments