VYUO vikuu nchini vimeagizwa kuwa chachu ya ufanikishaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais John Magufuli ya kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
Hayo yamesemwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizindua Kongamano la Elimu ya Juu na Tanzania ya Viwanda katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Samia amesema, ili serikali iliweze kufikia malengo yake inahitaji kuwa na wasomi wengi wenye elimu za juu ambao wataisaidia nchi katika kufikia uchumi wa viwanda kutokana na elimu ya uhakika waliyoipata vyuoni.
"Wakufunzi wetu wa vyuo mbalimbali nchini wanapowaandaa vijana wetu katika masomo yao basi iwe pia ni chachu ya ufanikishaji wa maendeleo kwa taifa kutokana na kile wanachokipata kutoka kwenye vyuo vyao," alisema Samia.
Aliwataka wanavyuo nchini kuondokana na dhana ya kuitegemea serikali katika kupata ajira na badala yake wajikite katika kujiajiri ili nao waweze kuwaajiri Watanzania wenzao na kuongeza kuwa serikali ipo tayari kuwasaidia wenye nia ya kuanzisha viwanda kwa kuwatafutia masoko na fursa nyingine.
Makamu wa Rais Samia alitumia muda huo kukipongeza Chuo Kikuu Huria (OUT) kwa kutawanya elimu katika maeneo mengi nchini ili Watanzania waweze kujiendeleza kielimu na si kubaki na elimu waliyonayo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthoni Mtaka alimpongeza Makamu wa Rais kwa hatua yake ya kushiriki katika kongamano hilo lenye kulenga ufanikishaji wa viwanda kupitia elimu ya juu
0 Comments