SIRI YA UFAULU BORA KIDATO CHA NNE 2017- MARIAN BOYS


MWANAFUNZI bora wa Kidato cha Nne 2017, Filson Mde wa Shule ya Sekondari ya Marian Boys ya Bagamoyo, mkoa wa Pwani, amesema ameshika nafasi hiyo kutokana na usikivu, nidhamu na kuwasumbua walimu wake mara kwa mara ili wamwelekeze masomo asipoelewa.

Akizungumza kwa njia ya simu na HabariLeo kutoka nyumbani kwao Kasulu, Kigoma, Filson alisema, tangu alipoanza kidato cha kwanza amekuwa akiwasumbua walimu wamwelekeze pale anapokuwa hajaelewa kitu darasani mwake. Alisema kutokana na hali hiyo, amejikuta akiwa anaelewa vitu vingi na mwisho wake amekuwa hana wasiwasi muda wa kufanya mitihani yake ikiwemo mtihani wa mwisho alioibuka kidedea.

Alisema, hajawahi kusoma masomo ya ziada na badala yake amekuwa makini katika kufuatilia masomo muda wa kawaida wa darasani. Aliwashauri wanafunzi wenzake kutambua kuwa ili wafanikiwe kwenye masomo, wanatakiwa kujipanga kusoma tangu mwanzo wa mwaka. Akizungumzia mikakati ya baadaye alisema anataka kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu na ndio maana alichagua masomo ya mchepuo wa sayansi amabayo ni Fizikia, Baiolojia na Kemia (PCB).

Mama yake mzazi, Elizabeth Ndabatinye alisema mwanaye alianza kufanya vema katika masomo na mitihani tangu akisoma Shule ya Msingi Amani, Kagera akishika nafasi za juu . Alisema alifahamu fika mwanaye angeshinda mtihani lakini hakuwahi kufikiria kuwa angekuja kuwa mwanafunzi bora ilivyotokea.

“Kweli ninamshukuru Mungu kwa kuwa huyu kijana tangu mdogo kweli amekuwa akifanya vyema na tena vyema sana na leo amewakilisha vema Mkoa wa Kigoma yaani Waha leo tuna raha kutoa Tanzania One ni furah,”alisema. Alisema kijana huyo ni wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto wanne. Wa kwanza ni Stamili kisha Filson, Marick na wa mwisho ni Enri.

Mkuu wa Shule ya Marian Boys, Ihonde Joseph alisema Filson amekuwa akifanya vema tangu alipoanza kidato cha kwanza na kuwa walimu walikuwa wakitarajia kuwa angefanya vema. “Kweli tulijua angekuja kuwa mmoja kati ya wanafunzi ambao wangefaulu kwa daraja la juu na tuliposikia amekuwa bora Tanzania nzima imetufurahisha, “alisema Mwalimu Joseph.

Naye mshindi wa pili kitaifa, Elizabeth Mangu alisema siri kubwa ya matokeo aliyoyapata ni kumwomba Mungu muda wake mwingi na jitihada alizokuwa amezielekeza katika masomo wakati wote alipokuwa shuleni hapo. Alisema aliamini bila Mungu hakuna kitu kinachoweza kufanyika ikiwemo kufanya vizuri katika mitihani yake hatua iliyompelekea kujiamini muda mwingi hadi jana alipopokea matokeo yake ya mtihani huo akiwa amefaulu.

“Nawausia wanafunzi wenzangu walio shuleni kuongeza bidii muda wote huku wakimtumaini Mungu kwa kuwa ndiyo kila kitu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu,” alisema Elizabeth. Alisema matarajio yake ni kuwa Mhandisi Mungu akimsaidia kufanya vyema masomoni.

Mama mzazi wa Elizabeth aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwalimu akifundisha katika Shule ya Sekondari ya Kilolezi Jijini Mwanza, alimshukuru Mungu akisema ameyapokea matokeo hayo kwa moyo mkunjufu na zaidi anamwombea mtoto wake azidi kufanya vyema.

Alisema Elizabeth ni mtoto wake wa pili kuzaliwa akitanguliwa na kaka yake anayesoma utabibu Chuo cha Uuguzi Sengerema, Mwanza. Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu ,Anna Mshana naye alisema siri ya kufanya vyema katika mtihani huo ni kujituma na kujiwekea malengo akitumia muda mwingi kumwomba Mungu awapo shuleni hapo na hata nyumbani.

Alisema malengo yake ni kuwa Msanifu Majengo Mungu akimsaidia huku mzazi wake ambaye ni Mwalimu Shule ya Sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam, Benjamin Mshana akieleza kupokea matokeo hayo kwa furaha. “Namshukuru Mungu, mimi ni Mwalimu wa Sayansi, muda wote nilikuwa naomba mwanangu aige kupenda masomo ya Sayansi, kaenda mbali na kunistaajabisha kwa kufanya vizuri zaidi kitaifa, ni jambo la kumshukuru Mungu,” alisema Mwalimu Mshana jana.

0 Comments