SERA YA ELIMU IMEPATWA NA KIHARUSI?


Sera yetu ya elimu imepatwa na kiharusi?

     

Kwa ufupi

Kabla ya kuzinduliwa, utekelezaji wa sera hiyo tayari ulikuwa umeshaanza kwa wanafunzi waliokuwa wameingia darasa la kwanza mwaka 2015.

Februari 13 mwaka 2015, Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alizindua sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014.

Kabla ya kuzinduliwa, utekelezaji wa sera hiyo tayari ulikuwa umeshaanza kwa wanafunzi waliokuwa wameingia darasa la kwanza mwaka 2015.

Kuanza kutumika kwa sera hiyo kulifanya kuandaliwe mtalaa wa elimumsingi darasa la I-II na utayarishaji wa vitabu vyake.

Kimsingi, sera yetu mpya ya elimu ina mitalaa miwili; wa elimumsingi darasa la I-II na wa elimumsingi darasa la III-VI. Mitaala hiyo miwili ikazalisha mihutasari mipya.

Sera imeelekeza muundo mpya wa elimu ya msingi kuishia darasa la sita badala ya darasa la saba. Sera pia imeelekeza shule ya msingi iwe na ngazi tatu za upimaji wa kitaifa.

Kuna upimaji wa darasa la pili, darasa la nne na darasa la sita. Sera mpya inaelekeza elimumsingi au elimu ya lazima kwa mtoto wa Kitanzania kuishia kidato cha nne.

Utaratibu wa uandaaji na utungwaji wa sera hapa nchini, unaelekeza utungwaji wa sheria mahsusi baada ya sera husika kutungwa ili sera hiyo iweze kutekelezwa. Kwa maana nyepesi sera iliyotungwa haiwezi kutekelezwa pasipo kutungiwa sheria.

Hali imekuwa tofauti katika utekelezaji wa sera hii, kwani utekelezaji wake ulianza pasipo kutungiwa sheria, hivyo kuleta mkanganyiko mkubwa katika shughuli za utoaji wa elimu na mfumo mzima wa elimu.

Hali hii imefanya mfumo wetu wa elimu uwe kama umepatwa na ugonjwa wa kiharusi.

Mkanganyiko kuhusu uandaaji vitabu, sintofahamu kuhusu muundo na kutoeleweka vizuri kwa dhana ya elimu bure na taratibu za michango shuleni ni sehemu tu ya mkanganyiko wa utekelezwaji wa sera hiyo.

Mkwamo ukitokea hakuna sheria ya kufanyia rejea ili kupata suluhisho, badala yake hisia za watu binafsi zimekuwa zikitumika.

Mihutasari ya darasa la kwanza na pili ilitayarishwa kwanza na baadaye uandaaji wa vitabu vyake.

Lakini uandaaji wa vitabu hivi ulipogubikwa na dosari nyingi, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ikasitisha matumizi ya vitabu hivyo na kuelekeza kuendelea kutumika kwa vitabu teule vya kampuni binafsi. Cha ajabu wizara haikusitisha matumizi ya mihutasari iliyotokana na sera mpya.

Wakati matayarisho ya vitabu vya madarasa mengine yakiendelea, darasa la pili lililoanza na vitini kuziba pengo la vitabu vya mtalaa mpya, likarudishwa kutumia vitabu vya zamani vilivyochapishwa na kampuni binafsi kwa mtalaa wa zamani.

Machapisho ya vitabu vya mtalaa wa darasa la tatu mpaka la sita na urekebishaji wa vitabu vya mtalaa wa darasa la kwanza na la pili kulingana mitaala mpya ya elimu yetu, ikapata pigo jingine baada ya kugundulika kuwa vitabu bado vina kasoro nyingi.

Waziri husika akachukua hatua haraka pamoja na kuliahidi taifa ndani ya Bunge kuwa atahakikisha kasoro zinarekebishwa, ili watoto wetu wapate vitabu bora. Kasoro zimerekebishwa? Tunasubiri kujulishwa!

Sera yetu mpya ya elimu kwa kuelekeza elimu ya msingi kuishia darasa la sita badala ya darasa la saba hakujaeleweka si tu miongoni mwa wananchi wa kawaida, bali hata kwa watekelezaji mahsusi wa sera hiyo na wadau wa elimu.

Japo wizara ililitolea ufafanuzi kuwa mfumo unaotumika ni ule wa kuishia darasa la saba, ufafanuzi huo unaacha maswali mengi bila majibu

Swali kubwa linajitokeza hapa ni kuwa tunalipataje darasa la saba wakati mtalaa kamili ulishaandaliwa kuishia darasa la sita?

Maudhui ya kufundishia na kujifunzia kwa darasa hilo la nyongeza yatapatikana wapi? Tutarudi kutengeneza sera nyingine mpya tena na hivyo mitalaa mipya au tutaishonea ‘kiraka?’

Upimaji kitaifa wa darasa la pili, nne na sita haiyumkiniki kufanyika na kufanikiwa. Kwani licha Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufanya majaribio ya upimaji darasa la pili mwaka 2015 katika shule 66 ili kuona namna bora ya kuanza kufanya mtihani huo mwaka unaofuata, mtihani huo wa kitaifa wa darasa la pili haukufanyika.

Kama hitimisho la elimu ya msingi sio darasa la sita tena, ni wazi hatutokuwa na upimaji tamati wa darasa la sita kama tafsiri ya sera iliyo kuhusu mtalaa wa elimumsingi wa darasa la tatu hadi la sita.

Mitalaa imebadilishwa, mihutasari imeandikwa upya, vitabu vimeandikwa upya, walimu na maofisa wateule wamepewa mafunzo juu ya mtalaa mpya, majaribio ya upimaji wa kitaifa umefanyika. Yote haya yamefanyika huku ikiwa sera hiyo ikiwa haijatungiwa sheria

Haihitaji darubini kutambua kuwa sera yetu mpya ya elimu ina changamoto nyingi na kubwa kiasi imeshindwa kabisa kufanya kazi ipasavyo.

Muundo haufanyi kazi, upimaji haufanyi kazi, utekelezaji hauendani na mitalaa na mihutasari yake. Najiuliza elimu yetu imepatwa na kiharusi?

0 Comments