Kauli ya Mzee Mkapa kuhusu elimu ni sahihi ila imechelewa
By Gratian Mukoba
Kwa ufupi
Hakuna awamu yoyote ambayo sikuipazia sauti juu ya mwenendo wa elimu yetu. Kwa bahati mbaya mara zote sauti yangu iliendelea kuwa sauti ya mtu aliaye nyikani.
Kongamano la kitaifa la kuangalia mustakabali wa elimu yetu limechelewa. Nilikuwa kwenye uongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) tangu utawala wa awamu ya pili na nikastaafu utawala wa sasa.
Hakuna awamu yoyote ambayo sikuipazia sauti juu ya mwenendo wa elimu yetu. Kwa bahati mbaya mara zote sauti yangu iliendelea kuwa sauti ya mtu aliaye nyikani.
Mwandishi wa vitabu wa Marekani Zig Ziglar, aliwahi kusema: “Hakuna mtu awezaye kurudi jana akarekebisha makosa yake, ila kila mtu anaweza kuanza leo na akawa na kesho nzuri.’’ Kwa hili nasema kama Taifa tukubaliane kurudi kwenye meza ya kuchorea mustakabali wa elimu yetu.
Kuna watu ukiwasikiliza wanahangaika na elimu yetu kutotoa wahitimu wanaoweza kushindana na wenzao katika soko la ajira. Mimi natamani mhitimu ambaye atakua zaidi ya kulinganishwa au kushindanishwa na wengine katika soko la ajira. Natamani elimu yetu imtoe mhitimu ambaye atajipambanua bila kuonyesha vyeti vya uhitimu.
Anayeweza kumimina moyo wake wote kwa ari ya ajabu katika kuendeleza Taifa hili na hatimaye dunia nzima. Elimu yetu imepungukiwa na vitu vingi mno ambavyo kongamano likiitwa, vitaweza kuainishwa maana makala moja haiwezi kuvimaliza.
Elimu yetu naichukulia kama fimbo ya kutembelea iliyobebwa kichwa chini miguu juu hivyo kuifanya ishindwe kumudu lengo lake la kutuvusha kwenye utelezi.
Natamani kongamano hili liwahi na liruhusu maoni huru juu ya kutafuta majawabu ya ubora wa elimu yetu kwa mustakabali wa Taifa letu na huu utakuwa ni uzalendo kwa Taifa na dunia.
Mwaka 2005 nikiwa Rais wa CWT nilihudhuria mkutano wa shirikisho la vyama vya walimu duniani uliofanyika nchini Brazil.
Kwenye mkutano huo lilipitishwa azimio la kutambua ushoga na kutowanyanyapaa walimu mashoga. Sisi Waafrika tulipiga kura kupinga azimio hilo, lakini Wazungu walikuwa wengi na kwa wingi wao waliunga mkono hivyo azimio hilo kupitishwa. Baada ya kushuhudia mwenendo wa dunia nje ya bara letu, nilijua sisi Waafrika tunapaswa kujipanga kwa kutoa elimu sahihi ili kuvinasua vizazi vijavyo na zahama hii.
Kwa bahati nzuri tuliporudi Tanzania, nchi yetu iliitisha mkutano wa elimu na CWT tulialikwa.
Nilipopata nafasi kuchangia nilieleza kituko cha kuwatambua mashoga na kuwasihi waandaaji mitalaa waone namna ya kuingiza kipengele cha kusaidia wasomi wetu kujielewa na kupinga tabia na mienendo isiyofaa na inayopaliliwa na Wazungu.
Hata hivyo, mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia alikuwa waziri wa elimu alitumia muda mwingi kuponda na kujiapiza kuwa suala la ushoga Tanzania halipo na hata likija halitakuwa na madhara.
Baada ya miaka michache kupita, nchi zetu zilianza kushinikizwa kutunga sheria za kuruhusu ndoa za jinsia moja.
Kitakachookoa nchi zetu za Kiafrika na udhalimu wa kimataifa ni watu kupata elimu bora iliyosanifiwa na watu sahihi wanaojiruhusu kutulia na kuiona Afrika miaka mingi mbele, jambo linalotulazimu kuzinduka sasa na kuingia katika mjadala huu adhimu.
Ni kweli tumechelewa kwa kuwa tulipaswa kukaa siku nyingi na kutafakari kuhusu mwelekeo wa elimu yetu. Hata hivyo, kuchelewa hakumaanishi hatuna haja ya kukaa. Tuifanyie kazi kauli ya Mkapa kuokoa elimu ya Tanzania.
Gratian Mukoba aliwahi kuwa rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT). 0754516612
0 Comments