WALIMU 50 WANIGERIA KUFUNDISHA ZANZIBAR


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali inatarajiwa kupokea walimu 50 wa masomo ya sayansi, ikiwa ni moja ya mikakati yake kuhakikisha wanafunzi wanafaulu vizuri masomo hayo.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri, amesema hayo wakati anatoa taarifa za mikakati ya wizara katika kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.

Ameyataja masomo yenye upungufu mkubwa wa walimu kuwa ni fizikia, baolojia pamoja na kemia ambayo ufaulu wake katika kipindi cha miaka mitano sasa ni mdogo.

''Napenda kutoa taarifa kwamba Wizara ya Elimu inatarajiwa kupokea walimu 50 kutoka Nigeria kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi ambapo 16 tayari wamewasili juzi,” alisema. Amesema, walimu 26 wanatarajiwa kuwasili Zanzibar hivi karibuni watakaofundisha kwa mkataba wa miaka miwili.

“Hiki ni kipindi cha tatu sasa Wizara ya Elimu tunapokea walimu kutoka Nigeria ambao kwa mujibu wa tathmini yetu, wameleta maendeleo makubwa kwa wanafunzi wetu,” alisema. Kiongozi wa msafara wa walimu hao, Profesa Afo Labi, alisema wamejizatiti kufundisha katika masomo ya sayansi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

“Tumejipanga vizuri kuona wanafunzi wanasomeshwa masomo ya sayansi na kufaulu vizuri ili wawe wataalamu na mabingwa wa baadaye,” alisema.

Mwishoni mwa wiki Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alikutana na Balozi wa Nigeria nchini Tanzania, Dk Sahabi Issa Gada Ikulu na kufurahishwa na uhusiano uliopo kati ya nchi hizo hususan katika kuimarisha sekta ya elimu ya sayansi.

0 Comments