MBUNGE ATAKA WALIOISHIA DARASA LA SABA WATIMULIWE BUNGENI


Mbunge wa Geita vijijini, Joseph Kasheku maarufu Musukuma, ameitaka serikali irudishe kazini watumishi wa darasa la saba iliowafukuza vinginevyo wabunge wenye elimu ya darasa la saba pia waondolewe bungeni.

Musukuma amesema hayo bungeni Mjini Dodoma leo Ijumaa Aprili 6, alipokuwa akichangia hotuba ya ofisi ya Waziri Mkuu.

Amesema wabunge wakishaondolewa bungeni warudishwe kwa Viti Maalumu kama ilivyo kwa wanawake na walemavu ili wawatetee darasa la saba wenzao.

Musukuma amesema hotuba ya Waziri Mkuu inaonyesha mwaka wa fedha uliopita waliojiunga na darasa la saba ni milioni mbili na walioingia sekondari ni 500,000 jambo linalomaanisha wenye elimu ya darasa la saba ni zaidi ya asilimi 80.

“Serikali isiposikia kilio chetu na kuwarudisha kazini watumishi hao na wabunge wa kambi zote kuungana na kutetea watumishi hao waliofukuzwa kazi basi tutakutana 2020,” amesema Musukuma

0 Comments