TRA YATOA ELIMU YA MLIPAKODI - GEITA


 Afisa wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) George Haule (kushoto) akitoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wakati wa Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani hapa na inatarajia kumalizika tarehe 13 Aprili, 2018.
 Afisa wa Kodi Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Maternus Mallya (kulia) akitoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wakati wa Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani hapa na inatarajia kumalizika tarehe 13 Aprili, 2018.
 Afisa wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Adela Kayella akimuhudumia mfanyabiashara aliefika kwenye Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani Geita. Kampeni hiyo inatarajia kumalizika tarehe 13 Aprili, 2018.
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakipita katika maduka mbalimbali kutoa elimu ya masuala yanayohusu kodi wakati wa Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani Geita. Kampeni hiyo inatarajia kumalizika tarehe 13 Aprili, 2018.


Wafanyabiashara na wananchi wa Mkoa wa Geita wamejitokeza kwa wingi kupata elimu ya mlipakodi inayoambatana na usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na kupatiwa makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara mbalimbali.

Akizungumza baada ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi wa Wilaya ya Bukombe na Mbogwe wakati wa Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani hapa, Afisa Kodi Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Maternus Mallya amesema mwitikio wa wananchi ni mkubwa na unaridhisha.

"Nimefurahishwa sana na mwitikio wa wananchi wa Mkoa wa Geita kwasababu wengi wameonyesha kiu ya kupata elimu na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na mpaka sasa takribani wafayabiashara 200 wamesajiliwa na kupatiwa namba hiyo pamoja na kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato," alisema Mallya.

Nae mfanyabiashara wa kuchomelea mageti wa Wilaya ya Bukombe, Mandela Alex amesema kuwa, amefurahishwa na ujio wa kampeni hii wilayani kwake kwani biashara yake imetambulika na kuingizwa kwenye mfumo rasmi wa kibiashara.

"Kwakweli mimi nimefurahi sana kupata namba hii ya TIN na sasa biashara yangu ni halali na imeingizwa kwenye mfumo rasmi wa kibiashara na nitalipa kodi kulingana na makadirio niliyopewa na watalaam wa TRA," Alisema Alex.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa vinywaji wa Wilaya ya Mbogwe mkoani hapa Beatha Kalungula ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Wilaya hiyo ambao hawajapata elimu na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi wafanye hivyo ili waweze kuwa na uelewa kuhusu kodi mbalimbali na biashara zao ziweze kutambulika.

"Mimi nimenufaika sana na elimu iliyotolewa hapa lakini pia nimefurahi mno kupata TIN namba ambayo itaniwezesha hata kupata mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kibenki ambazo moja ya vigezo ni kuwa na TIN namba ya biashara yako, hivyo nawaambia wafanyabiashara wenzangu ambao hawajafika hapa, waje wakutane na wahusika wa TRA kwajili ya kupata elimu ya kodi na kujisajili kama mimi nilivyofanya," alifafanua Beatha.

Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi mkoani Geita itamalizika tarehe 13 Aprili, 2018 ambapo pamoja na mambo mengine, wafanyabiashara wapya wanasajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kodi na manufaa yake kwa Taifa.

0 Comments