IN SUMMARY
Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imemkabidhi tuzo maalumu mwalimu Magreth Lubelege aliyewezesha madarasa ya watoto watukutu walio gerezani kufaulu vizuri katika mitihani yao ya darasa la saba kwa kipindi alichokuwa akifundisha kabla ya kustaafu.
Mwalimu huyo aliyeanza kufundisha gerezani tangu mwaka 2003, amekabidhiwa tuzo hiyo ili kutambua mchango wake katika kuinua sekta ya elimu hasa kwa watoto walioonekana kama wameshindikana.
Mbali na mwalimu huyo, shule mbalimbali za manispaa ya Ilala zizofanya vizuri kwenye mitihani ya darasa la saba ya mwaka jana, pia zimepatiwa tuzo.
Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Ilala, Elizabeth Thomas amesema mwalimu Lubelege amepewa tuzo baada ya kumudu kuwafundisha watoto hao na kuwawezesha wengi wao kufikia elimu ya juu japo walionekana watukutu.
“Hata kama amestaafu mchango wake ni mkubwa na hatuna budi kumkabidhi tuzo hii tukitambua mchango wake katika kuwafundisha watoto wetu ambao walionekana kuwa wameshindikana,” amesema Elizabeth.
Shule kumi bora za Serikali za Manispaa hiyo zilizopewa tuzo ni Mtendeni, Zanaki, Kiwalani, Msimbazi Mseto, Diamond, Lumumba, Msimbazi, Mkoani na Maktaba.
Pia shule binafsi zilizofanya vizuri na kupewa tuzo hiyo ni kuwa Lusasaro, Fountain Gate, Tusiime, St Joseph Millenium, Gerious King, Motivale, Heritage na Green Hill.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo, Mwalimu Lubelege alisema sio rahisi kuwafundisha watoto wanaoonekana kuwa ni watukutu.
0 Comments