ELIMU YETU IELEKEE KWENYE UCHUMI WA VIWANDA

Kama kawaida yetu Watanzania, wapo waliobeza zoezi hili kwa sababu za kisiasa zaidi, pinga kila kitu. Pamoja na hatua hii kumalizika huku kukiwa na malalamiko kuwa bado wenye vyeti vya kughushi wapo kazini, matokeo yake yametuonyesha wazi kuwa tuna haja ya kuiangalia elimu yetu kwa jicho la pili.
Idadi ya waathirika wa vyeti vya kughushi ni kubwa huku kukiwa na hisia kuwa wengi bado wapo serikalini. Aidha, mpango huo haukugusa mashirika ya watu binafsi ili kutupa picha halisi ya ukubwa wa janga hili.
Bila shaka iwapo eneo hili lingeguswa, tungeona wangapi wana vyeti visivyokidhi matakwa ya elimu wanayodai wanayo. Nina imani wanataaluma watalifanyia utafiti na kutupa majibu siku moja.
Suala la elimu bora na si bora elimu limekuwa ni nguzo katika mageuzi yote ya kiuchumi hapa duniani. Tanzania imeamua kuingia katika uchumi wa viwanda tukiwa na maana ya kujenga au kuanzisha viwanda vya aina mbalimbali na kuajiri Watanzania kufanya kazi za uzalishaji katika viwanda hivi.
Ni wazi kuwa mahitaji ya wafanyakazi yatakuwa katika kada mbalimbali, hivyo kuwa na uhitaji wa elimu katika viwango mbalimbali pia. Kwa kuzingatia ukweli huu, utaona ni kwa nini Rais Magufuli aliamua kuanza kwa kuonyesha thamani ya elimu na si sifa ya elimu.
Ebu tujifunze kutokana na mafanikio waliyoyapata baadhi ya Watanzania na wawekezaji wageni kupitia viwanda vilivyopo hapa nchini. Nawazungumzia akina Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa, Dangote, Simba Cement, Murza Oil, kwa uchache, wanatushauri nini kuhusu mchango wa elimu katika mafanikio waliyoyapata.
Hapa sina maana elimu waliyonayo wamiliki wa viwanda hivi, bali elimu inayotakiwa katika uendeshaji na usimamizi wa viwanda vyao. Wameajiri wageni wangapi katika nafasi zinazohitaji elimu na utaalamu fulani ambazo Watanzania wana elimu hiyo au sifa hizo? Lazima kuna sababu iliyowasukuma kuchukua maamuzi hayo.
Ninachelea kusema kuwa kama hatutalipa umuhimu suala la elimu bora kwa Watanzania si ajabu tukaishia kujenga viwanda na kufaidisha nguvukazi ya nje huku Watanzania wengi tukiendelea na kazi za ‘sulubu’ katika viwanda hivyo.
Hapa inabidi nirudie usemi nilioutumia hapo juu kuwa elimu inatakiwa kuwa bora na si bora elimu. Tunapozungumzia kufaidika na viwanda vyetu kwa kutoa nguvukazi watu yenye ubora wa kupata ajira katika kada za kitaalamu na zenye malipo ya juu, inahitajika elimu bora kwani huenda elimu mbovu ikawa sawa na suala la kughushi vyeti.
Aliyeghushi cheti atakataliwa kama ambavyo atakataliwa mwenye cheti cha kweli lakini ana uwezo mdogo wa kiutendaji kutokana na ubovu wa elimu aliyoipata.
Elimu haina siasa na ubora wake hupimwa kupitia uwezo wako katika utendaji na unapozungumzia ubora wake – Ni uwezo wa kutenda na kutoa majibu kwa matatizo yaliyopo.
Kwa mtazamo wangu, hili ndilo suala ambalo Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako amekuwa akilipigania. Anataka kuipa elimu ya Tanzania tafsiri ya dunia nje ya siasa.
Yaani anataka iwe elimu itakayotupa heshima ndani ya viwanda vyetu na katika sehemu zetu za kazi, ni elimu itakayotoa majibu ya matatizo yetu.
Tunataka elimu ya ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa viwanda kama wataalamu na siyo vibarua. Tuendelee na hili bila kukatishwa tamaa na kelele za kisiasa. Wekezeni katika elimu bora, maana cheti feki na elimu mbovu ni ndugu wamoja.
Ad 

0 Comments