Kwa ufupi.
Machi 17, 2018 ilikuwa ni siku muhimu kwa wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), ambao kwa mara ya kwanza walishuhudia sura mpya ya uongozi wao tangu kuanzishwa kwake miaka 11 iliyopita.
Hata hivyo, sherehe za wasomi hao ziliambatana na huzuni na vilio kwa baadhi ya watumishi hasa lilipotajwa jina la Profesa Idrisa Kikula kwamba anastaafu rasmi utumishi katika taasisi hiyo.
Haikuwa mara ya kwanza kwa Kikula kustaafu, lakini ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kuaga, kwani mara zote amekuwa akistaafu na kurudishwa kwa mkataba. Safari hii kiti chake kilipata mkaliaji.
Tarehe hiyo itakumbukwa kwa kupishana katika kiti kati ya Profesa Idrisa Kikula na Profesa Egid Mubofu ambaye anachukua kijiti hicho kuendeleza harakati za chuo, ambacho lazima nikiri kuwa uwepo wake umesaidia kuibadilisha sura ya mji wa Dodoma.
Kwa hakika mwenye macho na masikio atakubali akisikia sauti ikisema ‘hongera Kikula kwa utumishi’ ama kweli umepigana na kweli umeshinda kwa kiasi chako, unastahili kupumzika.
Profesa Kikula anaondoka Udom ikiwa na wanafunzi zaidi ya 25,000 katika kipindi cha miaka 11 kutoka wanachuo 1200 alioanza nao mwaka 2007, huku lengo la Udom likiwa ni kudahili wanafunzi 40,000.
Mengi ameyafanya Profesa Kikula, lakini kubwa litakalokumbukwa ni jinsi alivyofanikiwa kuzuia maandamano yaliyokuwa yanatikisa kwa kiasi kikubwa mji wa Dodoma na kutishia kufungwa kwa chuo.
Si hivyo tu, msomi huyo atakumbukwa kwa kuijenga taasisi hiyo kutoka msitu na kuwa kama halmashauri inayovutia madhari ya Dodoma, huku akijenga ujirani mwema na wakazi wa vijiji vya Iyumbu, Ntyuka, Dodoma Makulu, Mapinduzi na Nghonghona.
Anaondoka huku Udom ikiwa na hospitali ya mfano iliyojaa mabingwa wa tiba.
Matarajio ya wengi ni kuona mrithi wa kiti akiwa na sifa hizi na hata za ziada ili Udom izidi kuchanja mbuga. Ni kweli kila zama na kitabu chake, bado tuna matumaini makubwa na ujio wa kiongozi mpya.
Kazi kubwa unayopaswa kuanza nayo Profesa Mubofu ni kuzuia siasa ndani ya chuo hicho ambazo awali zilitamalaki kwa kiasi kikubwa.
Mtangulizi wako aliweza kudhibiti na alifanikiwa, licha ya kuwa kwa sasa zinarudi kinyumenyume kwa kupitia vyama viwili vikubwa; liangalie hilo kama mboni ya jicho lako.
Profesa Mubofu unapaswa kufanya kazi ya ziada katika kulinda mazingira ya chuo kwa ujumla, kwani bado kuna watu wanalinyemelea eneo hilo kwa ajili ya kuchunga mifugo yao na wengine kujitafutia nishati mbadala.
Misitu iliyotunzwa na mtangulizi wako itakuwa na maana na faida kubwa ya kufanya eneo hilo kubaki na uasili wake ikiwa mtaweka sheria ndogo na kuziishi.
Hata hivyo, epukeni kuondoa miti ya asili na kutaka kupanda ya kisasa kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa mmeiondoa heshima ya Udom.
Hapana shaka Profesa Mubofu anatambua kuwa hicho ni chuo kikubwa kuliko vingine katika ukanda wa Afrika Mashariki kinachotegemewa kuzalisha wasomi na viongozi tarajali.
Bado kuna ramani ambazo mtangulizi wako alishaanza kuzifanyia kazi ili ndoto yake ya kuwa na taasisi ya mfano iweze kutimia, sijui kama utafanikiwa kuziendeleza au kama utaingia na ndoto zako nzuri kuliko hizo kwa manufaa ya Wana- Udom.
Kama haitoshi, hapo ni mahali pekee unapoongoza wasomi wasiokuwa na kona kwani uhakika wa vyeti ulithibitisha hilo kwa chuo kizima kupatikana wahudumu wa kada ya chini wawili tu kwamba ndiyo walikuwa na vyeti bandia, huku wasomi wote wakionekana kuwa safi. Hongereni Udom.
Lakini kuchaguliwa kwa Mubofu kunaweza kuwa na maana kubwa kwani alingojewa kwa hamu mtu anayeweza kuvivaa viatu vya Kikula ndiyo maana awamu mbili zote alistaafu na kurudishwa ili aandaliwe huyo ajaye na sasa amefika.
Mubofu uje na ubunifu mpya kwa manufaa ya chuo. Miongoni mwa mambo unayoweza kusisitiza ni Udom kutoa kozi za masomo ya jioni kama ilivyo kwa washindani wenu.
Kazi za tafiti na kozi mbalimbali za ushirikiano alizoanza nazo mtangulizi wako, ni muhimu kuzidumisha na kuboresha ili kuwa katika ushindani wa kitaalumu unaotakiwa.
Ujio wa makao makuu uwe chachu ya kukiendeleza chuo ambacho awali mtangulizi wako alikitoa kikiwa msituni. Jitahidi kuondosha kero kadhaa ikiwamo kuachana na ofisi za wizara ili kuzuia mwingiliano.
Naamini bado chuo kina majukumu mengi yanayohitaji wahusika kuwa na maeneo ya kufanyia kazi.
Itoshe sasa maeneo ya chuo hicho kutumika kama hifadhi kwa vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali zilizohamia Dodoma baada ya uamuzi wa Serikali kuhamia katika mji huo.
0 Comments