MWANAFUNZI Daniel Wanje (22) amepata ufadhili kutoka mwanzilishi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) baada ya kutangaza katika vyombo vya habari kusudio la kutaka kuuza fi go moja ili apate fedha za kulipia masomo yake ya elimu ya juu.
Wanje, alifanya mtihani wa Cheti cha Elimu ya Sekondari (KCSE) mwaka 2015 na kupata alama ya B+ lakini kutokana na kukosa Ada alishindwa kujiunga na Chuo kikuu. Mwanzilishi na Mwenyekiti wa MKU, Profesa Simon Gicharu baada ya kusikia tangazo hilo aliamua kumsaidia.
“Profesa Gicharu amenipa ufadhili wa mwaka mmoja, ikihusisha ada ya mafunzo, bweni pamoja na fedha ya kujikimu,” alisema Wanje “Nilimaliza sekondari katika Shule ya Wavulana ya Ribe na kupata alama ya B+ lakini kutokana na kukosa fedha nilishindwa kujiunga na chuo kikuu kama nilivyotarajia, nimekaa kwa mwaka mmoja na kuamua kuuza figo kwa ajili ya kupata ada,” alisema Alisema familia yake haikumuunga mkono, lakini hawakuwa na njia mbadala, hivyo walikubaliana naye kwani hawakuweza kumpatia fedha za kujiunga chuo kikuu.
“Nikiwa natafuta mnunuzi wa figo katika vyombo vya habari, Profesa Gicharu alinitafuta na kuahidi kunilipia masomo yangu na baada ya kupata ufadhili huo, nimejisikia vizuri na sikuamini mpaka nilipodahiliwa chuoni,” alisema Alishauri wanafunzi wengine wanaotoka katika familia zisizojiweza kutokata tamaa na wasione aibu kwenda katika jamii kuomba msaada, kwani hata yeye anaendelea kuomba wafadhili kumsaidia masuala mengine kwa ajili ya miaka mingine ya masomo yake
0 Comments