WASOMI WAHIMIZWA KUANDIKA VITABU




Rai imetolewa kwa wasomi nchini kujenga utamaduni wa kuandika vitabu vya aina mbalimbali vitakavyoelimisha jamii kuhusu uendelezaji wa viwanda na fursa za maendeleo ili wananchi wafahamu mengi juu ya nchi yao.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi ametoa rai hiyo pia akahimiza watanzania kujenga tabia ya kujisomea mara kwa mara, wakati akizindua kitabu cha ‘Uchumi wa Viwanda’ kichoandikwa na Mhandisi wa Ujenzi, Yuda Kamencha, leo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Abbas amesema vijana wanatakiwa kutumia elimu na kujikita katika kuandika vitabu hasa vinavyoelewesha wananchi kuhusu uwekezaji katika sekta ya viwanda na kuwa ndio sera kipaumbele ya Serikali ya Awamu ya Tano ikusudiayo kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini.

“Wasomi wetu wengi ni walalamishi, watu wa kuhamisha nadharia za ulaya, hawaandiki vitabu wala hawafanyi utafiti, hivyo tunaomba wasomi wajikite katika kuandika vitabu mbalimbali ili kutoa maarifa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine,” amehimiza Dkt. Abbasi.

Akipongeza juhudi za Mhandisi Kemincha, Dkt. Abbasi amesema Mhandisi amenyambulisha kwa lugha rahisi mahitaji halisi katika kufanikisha sekta ya viwanda nchini na kushauri aendelee na juhudi hizo kwa kujitolea muda wake na gharama kuandika vitabu vya kuhamasisha na kuelemisha watanzania.

Kwa upande wake Mhandisi Kemincha ameeleza kuwa katika kitabu chake amenyambulisha mahitaji halisi vya viwanda vyetu, “kwa mfano, mahitaji ya viwanda karakana ni muhimu kama ilivyo kwa aina zingine za viwanda” amesema Mhandisi.

Mhandisi Kemincha amempongeza Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za dhati zenye nia ya kuleta mapinduzi ya uchumi nchini kwa kasi kubwa, pia akampongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ushauri wake wa kuzindua kitabu hicho ili kiwafikie watanzania wengi.

0 Comments