Siku kadhaa baadaye, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete aliungana naye kuhusu matatizo ya elimu na kutaka mfumo uangaliwe.
Marais hao wastaafu ni mwangwi wa kelele za matatizo yaliyoko kwenye mfumo wa elimu Tanzania ambao wasomi na wanasiasa wanataka mfumo wake uangaliwe upya uende na wakati.
Wamekuwa wakidai wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu wanaacha maswali mengi kuhusu uwezo wao na kufanya waonekane hawajaiva. Tumeguswa na tatizo la elimu Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki (EAC) baada ya kuwepo habari za matatizo hayo nchini Kenya.
Kenya kuna habari za ukosefu wa wahadhiri wa kutosha wa shahada ya uzamivu (PhD) katika vyuo vikuu vya umma unaofanya wanafunzi wa shahada za juu kuchelewa kuhitimu.
Imeelezwa wahadhiri wachache waliopo wanasimamia wanafunzi wengi na kutokuwa makini na wanafunzi wa shahada ya uzamivu.
Kutokana na tatizo hilo, Baraza la Vyuo Vikuu vya Nchi za Afrika Mashariki (IUCEA) linapendekeza usimamizi kuwa wa wazi zaidi na msimamizi awe na wanafunzi wachache zaidi.
Ripoti inaeleza wahadhiri wenye PhD wanahudumia wanafunzi 94 badala ya 30 iliyopendekezwa na wataalamu wa elimu ya juu.
Hayo yanatokea wakati vyuo vikuu binafsi vikiwa vimetakiwa kupeleka taarifa ya mwaka ya fedha Tume ya Taifa ya Elimu ya Vyuo Vikuu Kenya (CUE) kukabili ukata na matatizo ya kiutawala.
Bodi ya CUE pia inataka vyuo hivyo kutaja wamiliki wake ili ikitokea kufilisika viwajibike. Hatua hiyo inalenga vyuo vikuu binafsi 37 vinavyokabiliwa na changamoto mbalimbali za usimamizi imara ukilinganisha na vya umma.
Kwa jumla, elimu kwa nchi hizo imekuwa janga na hivyo iko haja EAC inapozidi kujiimarisha kuelekea shirikisho la kisiasa, ikaangalia hilo.
Tunasema EAC ivalie njuga elimu kwa sababu bila elimu, hakuna kitakachofanikiwa kwani kamwe haitapata rasilimali watu wenye weledi.
Ni vyema Tanzania, Kenya, Rwanda na nchi zote za EAC zenye matatizo na zisizo na matatizo ya mfumo wa elimu, zikatafuta suluhisho la pamoja la janga hilo.
Haina maana nchi moja ya EAC kujidanganya wasomi wake ni wazuri lakini wanapoingia sokoni, wanamezwa na wenye elimu duni.
Ni vyema EAC ikaitisha kongamano la wasomi na wadau wa elimu ya vyuo vikuu na mabaraza yake kujadili mustakabali wa elimu hiyo kwa EAC.
0 Comments