Jinsi ya Kukuza Biashara

Dar es Salaam. Waswahili wanasema polepole ndio mwendo na mtaka cha uvunguni sharti ainame. Hiyo ni misemo inayoakisi maisha ya Senkondo Mashaka (23), mlemavu wa mguu anayeeleza safari ya mafanikio yake kutoka kuwa winga na sasa anamiliki duka lake.

Mbali na duka hilo, Senkondo pia ni mfugaji wa kuku na anamiliki kampuni ya uwakala wa mizigo.

“Nilianza kuwa winga tangu nilipomaliza kidato cha sita mwaka 2020. Kazi yangu ilikuwa ni kufanya makubaliano na wafanyabiashara wenye maduka waliokuwa wananiuzia bidhaa kwa bei ya chini kisha nakwenda kuuza kwa bei ya juu kwa wateja,” anasema

Anaeleza kwamba mara nyingi mawinga wanakuwa karibu na wenye maduka na wakati mwingine wanasimama kama wauzaji wa maduka hayo, hasa anapokuwa amewapata wateja wengi.

Njia aliyokuwa akiitumia kupata wateja kama ilivyo kwa mawinga wengine ni kujitangaza na muda wote kuhakikisha anauza bidhaa zenye ubora kwa bei nafuu.

Akizungumzia changamoto alizopitia, Senkondo anasema zinaweza kupita siku mbili au tatu hujafanya mauzo na hakuna mteja aliyempata kiasi cha kukosa fedha za kujikimu.

Pia ameeleza kuwepo kwa wivu kwa wenye maduka makubwa, endapo winga amefanya mauzo mengi na kupata faida kubwa kuliko yeye.

“Wenye maduka wengi wanachukia pale jina la winga linapokuwa kubwa kuliko majina yao,” alisema.

Senkondo anasema mbali na kuwa na duka lake la vifaa vya simu, kazi ya uwinga imemsaidia kufungua miradi ya pembeni kama ufugaji kuku na kuwekeza katika kilimo cha mihogo.

“Kwa mafanikio haya niliyokuwa nayo watu sasa ndio wameanza kuamini kazi ya uwinga sio ya kudharaulika,” alisema.

Senkondo alifanya kazi hiyo licha ya kufaulu kwa daraja la kwanza alipohitimu kidato sita, kwa kuwa biashara zake zimeimarika sasa anasema anatarajia kujiunga chuo kikuu.

“Awali nilipata ufadhili wa masomo nchini Uturuki, lakini sikwenda, niliona nijikite kwenye biashara kwanza. Nashukuru sasa biashara zimesimama, nitasomea hapahapa nchini,” amesema.

Senkondo anawashauri vijana kuthubutu kitu kinachoweza kuwapa mafanikio na wasiwe waoga kuwekeza, kwani ni vigumu kufanikiwa ukiwa mwoga.

“Kila biashara ina changamoto na raha yake, hivyo vijana wasiogope kuwekeza na kuthubutu, maana mafanikio hayawezi kuja ukiwa mwoga. Ukithubutu utaona mambo yanenda,” amesema.

Felix Zakaria, aliyekuwa pia winga kwenye maduka ya nguo tangu mwaka 2018, kwa sasa anamiliki duka la nguo analosaidiwa na vijana wawili kulisimamia.

Akieleza safari yake, Zakaria anasema haikuwa rahisi, kwani alianza kwa kutumwa na wenye maduka.

“Kuna wakati watu walikuwa wananikatisha tamaa na nikicheki nilikuwa naingiza hela ndogo basi nilikuwa nachanganyikiwa kabisa hadi kutamani kuacha, lakini niliendelea,” anasema.

Kati ya changamoto alizowahi kukutana nazo, Zakaria anasema ni kutuhumiwa wizi katika duka moja alikokuwa anapeleka wateja, hali iliyomfanya ajisikie vibaya kabla mwizi halisi hajajulikana baadaye.

Changamoto nyingine anasema ni pale mteja anaponunua bidhaa halafu ikaharibika, hivyo lawama kuanzia kwake kwa kuwa yeye ndiye aliyempeleka dukani.

“Kuna kipindi ilibidi nitoe hela yangu mfukoni kutatua changamoto iliyomkuta mteja wangu ili kujenga uaminifu na mteja asipotee,” alisema.

Anasema watu wengi wana mtizamo tofauti kuhusu mawinga, wengine wakiamini ni wahuni na matapeli, jambo ambalo si kweli, kwani wapo wenye malengo kwamba, yeye alifanikiwa zaidi kutokana na makubwa aliyoyafanya mwaka jana.

“Mwaka jana ulikuwa wa neema kwangu, nilikuwa napata kati ya Sh200,000 hadi Sh300,000 kwa siku kutokana na uaminifu nilioweka kwa wateja na wauzaji wa maduka,” amesema.

Kutokana na mafanikio hayo, Zakaria ameanzisha duka la nguo na anasisitiza: “Ukiwa na malengo utafanikiwa.”

0 Comments

Newest