MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kupitia Chuo cha Veta Mikumi imeingia katika ushirikiano na Chuo cha NOVA Scotia Communinity College (NSCC) cha nchini Canada ili kubadilishana uzoefu katika teknolojia za kiufundi kwenye masomo ya wanafunzi na walimu wa pande hizo mbili.
Mkuu wa Chuo cha Veta Mikumi, Christopher Ayo alisema hayo mwishoni mwa wiki, wakati wa maonesho ya kazi za ufundi zinazofanywa na wanafunzi wa kozi mbalimbali zinazotolewa Chuoni hapo. Alisema kutokana na ushirikiano huo, Serikali ya Canada na Chuo cha NSCC wametoa Dola 36,000 za nchi hiyo zilizowezesha utekelezaji wa mradi wa maabara ya Kifaransa na Kiingereza, pamoja na ufungaji wa umeme wa jua katika majengo ya Veta Mikumi.
Alisema, fedha hizo zimewezesha pia kukamilishwa kwa mradi wa kusafisha maji ya kisima yenye chumvi kwa kupunguza kiwango kilichokuwemo. “Tumekuwa na ushirikiano na nchi ya Canada kupitia Chuo cha NOVA Scotia Communinity College, ni ushirikiano wa kimafunzo kwa wanafunzi na walimu ili kuwawezesha vijana wanapohitimu wawe na ujuzi wa kuajirika na hii ni pamoja na walimu wetu kupata maarifa mapya,” alisema Ayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Mashariki, Asanterabi Kanza, alisema Veta inakwenda na wakati kulingana na mabadiliko ya teknolojia sambamba na kuwa na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia wanafunzi. Naye Mshauri Mwandamizi wa Kiufundi na Mwakilishi wa vyuo na Taasisi za Canada katika mradi wa ushirikiano wa kulimalisha stadi zinazowezesha kuajirika zaidi (ISTEP), Dk Alan Copend alisema, mradi huo ni wa matumizi teknolojia katika kufundisha na kuandaa mitaala ya kumwezesha mhitimu kuajirika ama kujiajiri mwenyewe.
Ili kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kuwa taifa lenye uchumi wa viwanda, Copend alisema uwekezaji mkubwa wa teknolojia za kisasa na mitaala wezeshi katika vyuo vya ufundi stadi ni moja ya njia ya kukuza ujuzi kwa vijana wanaojiunga na vyuo hivyo kupata stadi za kutosha na za kisasa zitazakazo wasaidia kuajirika na wao kujiajiri, na hatua hiyo iende sambamba na kuweka mazingira mazuri vyuo vya ufundi vinavyotoa masomo ya diploma na shahada za juu
0 Comments