FUNGUO TANO ZA MAFANIKIO YA MJASIRIAMALI

Funguo Tano Za Mafanikio Ya Mjasiriamali Wakati Wote

Kitu kizuri kwa mjasiaramali yoyote yule uwe unaanza au tayari safari hiyo  ulishaanza ni kujiandaa kuwa mshindi. Ni muhimu sana kujua wewe ni mshindi kwa kile unachokifanya bila kujali ni changamoto zipi unakutana nazo.

Lakini hata hivyo huwezi kuwa mshindi kama hutaweza kujua siri ya ushindi huo utaupata vipi. Kutokana na hilo sasa hapo ndipo unalazimika kuzijua funguo tano za  mafanikio ukiwa kama mjasiriamali.

Hizi ni funguo tano kweli kwa mjasiriamali ambazo ukizitumia, zitakupa mafanikio na kukufikisha kule unakotaka kufika . Funguo hizo ni zipi, fuatana nasi katika makala yetu ya leo kujifunza.

1. Weka kushindwa nyuma kabisa.
Kwa kawaida huwa yapo makosa  na kushindwa kwingi hasa pale unapoanza biashara au hata pia unapokuwa unaendelea na biashara yako. Yote hayo yanapotokea ikiwa kweli wewe ni mjasiriamali uliyenuia hebu yasahau.

Kitu kukubwa kwako angalia kule unakokwenda. Makosa ni sehemu pia ya kukusaidia kufanikiwa kule unakokwenda ikiwa utajifunza. Acha kuamini kwamba utashindwa kirahisi. Amini utashinda kwa hicho unachokifanya.

2. Weka juhudi nyingi kila siku.
Anza siku yako kila siku kwa kujua kwamba unakwenda kuweka juhudi nyingi sana ambazo kwa vyovyote vile zitakuletea matunda. Jione mshindi kila iitwapo leo. Acha kujiona mnyonge.
Unapokuwa mjasiriamali unayejitambua ni lazima uelewe hili kwamba mafanikio yako yanategemea sana pia kutokana na juhudi unazoziweka. Hakuna kubahatisha ni kuweka juhudi ndiko kutakapokupa matokeo chanya.

3. Jifunze na jirekebishe kila siku.
Usiruhusu kutokujifunza, kila siku jifunze unapokuwa kwenye safari yako ya ujasiriamali. Kuna njia nyingi za kujifunza kama semina, mitandao na hata kutumia vitabu, hapo chagua njia iliyo bora kwako na ujifunze kila siku.

Kujifunza kunakusaidia sana kuchukua taarifa kutoka kwa wajasiriamali waliobobea kutoka sehemu mbalimbali duniani na kunakufanya na wewe kuzidi kuwa bora. Tumia muda hapo japo kidogo kujifunza na usiache.

4. Fuatilia biashara yako kwa ukaribu sana.
Ni vyema kutambua upo umuhimu wa wewe kuifatilia biashara yako kwa ukaribu sana kuliko unavyofikiri. Acha kufanya sana biashara yako kwa simu, kuwa karibu nayo.

Hata pale inapotokea umeajiri watu wengine, hiyo isiwe eti ndio basi kila kitu kimeishia hapo. Upo ulazima pia wa wewe kufatilia hatua zingine nazo kwa ukaribu zaidi kila wakati.

5. Kataa kushindwa mapema.
Kukutana na magumu katika kitu chochote ni jambo la kawaida. Sasa najua wewe ni mjasiamali mkomavu jipe ahadi kwamba hata ikitokea magumu vipi, kukata tamaa mapema  lisiwe jambo rahisi kwako

0 Comments