WASIOJUA KUSOMA NA KUANDIKA SERIKALI INASTAHILI LAWAMA


Mungu akitujalia, Desemba tutaadhimisha miaka 56 tangu tupate uhuru na kuwa taifa linalojisimamia na kujipangia mambo yake lenyewe.

Tutasherehekea miaka hii tukiwa na asilimia 23 ya Watanzania wasiojua kusoma, kuhesabu wala kuandika huku tukiwategemea kuhakikisha nchi yetu inapata maendeleo ya kiuchumi na kisayansi.

Takwimu zinaonyesha asilimia 23 ya Watanzania wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 54 ambao ni sawa na milioni 5.4 hawajui kusoma wala kuandika au kuhesabu.

Hadi sasa umri wa kustaafu kisheria ni miaka 60 hivyo kundi hili la wasiojua kusoma na kuandika bado ni nguvukazi inayohitajika katika maendeleo ya taifa letu.

Suala la jamii fulani kuwa na watu wasiojua kusoma na kuandika si la bahati mbaya bali linachangiwa na uzembe. Ni dhahiri wengi hatuoni umuhimu wa elimu ndiyo maana leo hii tunajikuta tupo tulipo.

Ipo mifano ya kutuouna umuhimu huu kwani hata sasa kuna shule zina wanafunzi 400 huku walimu wakiwa wanne ilhali nyingine hasa za mjini zina wanafunzi 200, lakini walimu ni 40 au zaidi. Endapo tungeona umuhimu wa elimu lazima kungekuwa na uwiano mzuri wa walimu kwa shule za vijijini na mjini.

Ujinga ni adui mkubwa wa maendeleo hivyo ni lazima tuonyeshe kwa vitendo kuwa hatutaki wananchi wetu waendelee kuwa wajinga kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kuondokana nao.

Serikali ilifanikiwa kuhamasisha upatikanaji wa madawati kwa shule zote za umma nchini. Watendaji kuanzia ngazi ya wilaya mpaka mkoa walihusishwa na madawati yakapatikana, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mikoa husika.

Kuna baadhi ya shule madawati yamepatikana, lakini hayana mahali pa kuhifadhiwa kutokana na uhaba wa madarasa. Vyumba vya madarasa havitoshi kukidhi hifadhi ya wanafunzi na madawati haya kwa ajili yao.

Tunahitaji uboreshaji wa mfumo mzima wa elimu kuanzia maslahi ya walimu na makazi yao, mazingira ya kazi, miundombinu ya shule na uhamasishaji wa jamii zisizo na msukumo wa elimu.

Ni aibu kuona shule ina matundu mawili au manne ya vyoo vinavyogombewa na walimu na wanafunzi wao kwani hali hii inasababisha utoro wa wanafunzi na walimu pia. Walimu wanayoyafahamu haya, huhakikisha hawapangwi huko.

Wakati hali ikiwa hivi, kuna kiongozi wa serikali anaendeshe gari inayozidi Sh200 milioni wakati ujenzi wa darasa moja ni wastani wa Sh30 milioni na nyumba ya mwalimu ikiwa haizidi Sh50 milioni.

Nasisitiza, bado hatujaona umuhimu wa kuboresha elimu yetu na siku tutakapouona tutachukua hatua. Kama gari ya kiongozi inapaswa kuwa ya gharama kubwa kiasi hicho ili aweze kuwafikia wananchi vijijini ambako barabara ni mbovu kutokana na uimara wake, ndiyo kipaumbele cha leo.

Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliwahi kusema ndiyo zana yenye nguvu zaidi unayoweza kuitumia kuubadili ulimwengu. Watanzania hatutaki kuitumia silaha hii kuibadili nchi yetu licha ya ukweli kwamba tunahitaji madaktari, wachumi na walimu tukielekea kwenye viwanda.

Hatuoni umuhimu wa elimu, ndiyo maana hadi leo Katiba inaruhusu mbunge awe anajua kusoma na kuandika tu. Bado tuna changamoto nyingi lakini tukiwa na jamii yenye elimu zitapungua kwa kiasi kikubwa.

Hakuna lisilowezekana na miaka 56 ya uhuru ni mingi kuendelea kuwa na wasiojua kusoma, kuhesabu au kuandika

0 Comments