Kwa ufupi
Jana katika gazeti hili kulikuwa na habari iliyoihusu Wakala wa Vipimo (WMA) mkoani Shinyanga kuendesha ukaguzi wa mizani ya kupimia pamba katika wilaya zote za mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa mauzo ya pamba.
Siku chache zijazo wakulima wa pamba katika mikoa inayolima zao hilo nchini wataanza kuuza mazao yao, hivyo WMA imeona ianze mapema kuwahakikishia upatikanaji wa kipato chao bila kuwa na hofu ya wanaowauzia kuwaibia kupitia mizani.
Kwa mujibu wa habari hiyo, tayari WMA mkoani humo imekwishakagua mizani 600 kati ya 2,000 ilizopanga kuzifikia mwaka huu, lakini sambamba na ukaguzi huo, wanakusudia kuondoa dhuluma waliyokuwa wanafanyiwa wakulima kwa kuwajengea uwezo wananchi wa maeneo hayo kwa ujumla kuitambua mizani inayofaa kwa biashara.
Meneja wa WMA mkoani Shinyanga, Elias Nyanda amekaririwa akisema kwamba wanafanya hivyo ili kuongeza tija kwa mkulima.
“Mizani zote zilizokaguliwa zina stika ili iwe rahisi kwa wakulima kuzitambua na kuruhusiwa kutumika kwa biashara kwa mwaka husika,” alisema.
Licha ya Shinyanga, inaelezwa kwamba elimu hiyo na uhakiki wa mizani pia inatolewa kwa wakulima wa mikoa mingine inayolima pamba ikiwamo Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Simiyu na Tabora.
WMA imekuwa na mikakati ya kumaliza dhuluma wanayofanyiwa wananchi katika mizani na wakati mwingine imekuwa ikipata msaada wa wanasiasa na viongozi. Mathalan, ni mara nyingi wakuu wa mikoa wamesikika wakipiga marufuku juu ya lumbesa, aina ufungashaji bidhaa na mazao ya wakulima ambayo ni ya kinyonyaji.
Ipo mifano mingi ya mikakati ya kudhibiti wizi huo unaowaumiza wakulima, ikiwamo ukaguzi wa magari yanayosafirisha mazao. Mikakati yote hii inayofanyika kwa lengo la kumsaidia mkulima, ni vyema ikaungwa mkono na kupongezwa.
Hata hivyo, suala la uhakiki wa mizani usiishie kwa wakulima hao tu kwani bado mwananchi au mteja wa kawaida aliyepo mtaani amesahaulika na hajapewa kipaumbele kumhakikishia haki yake kwa kile anachostahili baada ya kununua iwe sokoni au dukani kinachopimwa kwa mzani.
Tunasema hivyo kwa sababu mizani mingi, hususan ile inayopima bidhaa mitaani inatia shaka iwapo haimuibii mteja na kama ukaguzi wake unafanyika ipasavyo, ndiyo maana malalamiko ya wateja wa bidhaa za rejareja juu ya ujazo wanaopimiwa hayaishi.
Malalamiko hayo hayaishi kwa sababu watu wanadai kuibiwa, na hatujaona jitihada za kutatua tatizo hilo. Tumewahi kuripoti juu ya malalamiko ya wananchi kulalamikia kupunjwa na wauzaji wa rejareja wakiwamo wa nyama, bidhaa za madukani kama mchele, maharagwe na unga, lakini hatujaona jitihada za makusudi kushughulikia suala hilo.
Ni vyema WMA ikaanzisha utamaduni wa kutoa elimu kwa wananchi na kutatua malalamiko yao haraka kwa kuhakikisha kuwa mizani ya wafanyabiashara wote inakaguliwa na kuhakikiwa kila baada ya kipindi fulani na wananchi wanaelimishwa kuitambua iliyohakikiwa.
Hivi sasa mizani iliyokaguliwa ambayo inatumika kutolea huduma haifahamiki kwa wanunuzi wa bidhaa yaani wateja, hivyo wengi wao huishia kunung’unika na wachache kulalamika hadharani wakidai kuibiwa. Hili haikubaliki.
Tunawaomba watumishi wa Wakala wa Vipimo watoke ofisini waende mitaani kutoa elimu kwa wananchi ili pamoja na mambo mengine, wawaelimishe namna ya kuitambua mizani iliyohakikiwa na pia uwasilishaji wa malalamiko yao kwa taasisi husika iwapo watakuwa na dukuduku nayo.
0 Comments