MH MBATIA ASISITIZA MJADALA WAKITAIFA KUBORESHA ELIMU


I





SERIKALI imesema iko kwenye mchakato wa kuandaa mjadala wa kitaifa unaolenga kuboresha zaidi sekta ya elimu nchini.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda aliyasema hayo bungeni Dodoma jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi).
Mbunge huyo katika swali lake, alisema udhaifu katika sekta ya elimu nchini ni mkubwa na kwamba serikali haioni umuhimu wa kuwepo na mjadala wa kitaifa wa kuboresha elimu.
"Leo hapa bungeni, wabunge wengi wamekuwa wakihoji mambo ya uhaba wa walimu, nyumba za walimu, vifaa vya kufundishia, haya yote ni mambo mtambuka, serikali haioni kuna umuhimu wa kuwa na mjadala huu ili elimu yetu ikawa sawa, bora na shirikishi kwa wote? Alihoji Mbatia.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kakunda alimshukuru Mbatia kwa kurejea kauli iliyotolewa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuhusu haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa wa elimu. "Sasa hivi tuko kwenye mchakato wa kuandaa mjadala huu, naomba tushirikiane katika maandalizi haya," alisema.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga (Chadema) alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inatatua kero za upungufu wa madawati na walimu mkoani Tabora kutokana na ukweli kuwa kwa sasa mkoa huo unafanya vibaya kielimu.
Akijibu swali hilo, Kakunda alisema pamoja na changamoto zilizopo sio kweli kwamba kiwango cha elimu kimeshuka sana mkoani humo kwa kufanya vibaya kwenye mtihani.
"Kwa miaka miwili mfululizo Mkoa wa Tabora umekuwa juu ya wastani wa ufaulu kitaifa na kwamba kiwango cha elimu kimepanda. Hili ni jambo la kujivunia," alisema.

0 Comments