JELA MIAKA 30 KWA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI, TANGANYIKA.









MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, imemhukumu Ofisa Tabibu wa Zahanati ya Kasekese iliyopo wilayani Tanganyika, Martin Mwashamba (27) kifungo cha miaka 30 jela.
Ofisa Tabibu huyo amepewa adhabu hiyo baada ya mahakama kumtia hatiani kwa makosa ya kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 15, aliyekuwa akisoma katika Shule ya Msingi Kasekese.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Odira Amwol amesema, mahakama hiyo imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka pasipo kutia shaka yoyote kuwa mshtakiwa ndiye aliyetenda kosa hilo.
Upande wa mashitaka ulioongozwa na Mwanasheria wa Serikali, Gregory Mhangwa uliwaita mashahidi watano mahakamani hapo, miongoni mwao akiwa mwanafunzi mwenyewe huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi watatu.
Hakimu Amwol amesema mshitakiwa ametiwa hatiani kwa mujibu wa kifungu cha Sheria namba 130 (2) na kifungu cha Sheria 131(1) cha kanuni ya adhabu Sura namba 16 marejeo ya 2002.
Mwendesha mashitaka, Mhangwa amedai mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 2, mwaka jana katika kijiji cha Kasekese kilichopo wilayani Tanganyika mkoani humo.
Mshitakiwa aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea, pia ana wadogo zake watatu ambao anawasomesha.

0 Comments