WANAFUNZI 256 WAPATA MIMBA 2017/18- RUKWA





MKOA wa Rukwa kwa sasa una jumla ya kesi 256 zinazohusiana na mimba kwa wanafunzi wa kike wa shule za sekondari na msingi.
Akizungumza katika mkutano uliondaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara Kuu Maendeleo ya Jamii na Ofisi ya Mkoa wa Rukwa kwa madereva bodaboda kuhusu mimba na ndoa za utotoni, Kaimu Katibu Tawala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Abubakar Kunenge alisema idadi ya kesi hizo imepatikana kwa kipindi cha miezi tisa kwa mwaka 2017/18.
Aidha Kunenge alisema baadhi ya baba wa familia mkoani Rukwa wanadhani mimba za utotoni siyo tatizo na linafanyika bila kujali madhara yake.
“Suala la mimba za utotoni ni kosa kisheria na ukosefu wa haki ya mtoto ambalo lazima tulikomeshe mkoani kwetu,” alisisitiza.
Aidha dereva bodaboda Mkoani Rukwa, Ezekia Kalinga akichangia mjadala wa mimba za utotoni, amesema mazingira ya kusomea wanafunzi si mazuri kwa sababu baadhi ya mabinti wanasafiri umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni.
Kwa mujibu wa takwimu za polisi mkoani Rukwa, wilaya ya Nkasi inaongoza kwa kuwa na wanafunzi 106 ikifuatiwa na wilaya za Sumbawanga vijijini (58), Sumbawanga Mjini (56) na wilaya ya Kalambo ni wanafunzi 36.

0 Comments