Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza kuanza kupokea maombi ya mwaka wa masomo 2018/19 kuanzia leo hadi Julai 15, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa katika mtandao wa kompyuta wa HESLB jana ilieleza kuwa maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao ambao umefanyiwa maboresho na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM).
"Tunawataarifu watarajiwa wanufaika wa mkopo wapya na wa zamani kwa mwaka 2018/19 kuwa mfumo wetu wa maombi kwa njia ya mtandao utafunguliwa kuanzia Alhamisi Mei, 10 (leo) hadi Jumapili Julai 15, 2018," ilieleza taarifa hiyo.
Kadhalika, HESLB iliwataka wanufaika na watarajiwa wa mkopo kuzingatia mwongozo wa utoaji mkopo na ruzuku kwa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2018/19.
Sehemu ya maelezo ya mwongozo wa utoaji mkopo inasema waombaji wote wanakumbushwa kuhakikisha maelezo wanayoyatoa katika fomu ya maombi ya mkopo, yawe sawa na maombi ya udahili wa chuo.
Pia ilieleza kuwa namba ya mtihani wa kidato cha nne iwe sawa na iliyopo kwenye maombi ya mkopo na udahili wa chuo.
Kadhalika, bodi imewataka waombaji kuhakikisha nyaraka zote za maombi ya mkopo wanazowasilisha zimehakikiwa na mamlaka husika.
HESLB imetaka waombaji kuhakikisha vyeti vyote vya kuzaliwa na vifo na vingine vinathibitishwa na Mamlaka ya Vizazi na Vifo (RITA) au ofisa aliyechaguliwa, ili kuthibitisha uhalali huo.
"Hata hivyo, Ofisa Wilaya Ustawi wa Jamii (DSWO) anaweza kuidhinisha ripoti ya kifo cha mzazi kutoka kwa mamlaka ya kijiji au kata," ilisema taarifa hiyo.
Mwongozo huo pia uliwataka waombaji kuhakikisha taarifa kuhusu wazazi, walezi na mdhamini (kazi, anuani ya mwajiri, namba ya simu, anuani ya posta) ziwe kamili na sahihi.
"Waombaji mikopo ambao wazazi wao ni viongozi waliotajwa katika Kanuni ya Uongozi wa Umma, hawapaswi kuomba kwa Sheria ya Mwaka 1995," taarifa ilifafanua na kueleza zaidi:
"Vilevile waombaji ambao wazazi au walezi ni wamiliki wa biashara, mameneja wakubwa katika mamlaka zinazotambulika zenye usajili, hawaruhusiwi kuomba mkopo."
Sehemu ya mwongozi huo inawataka waombaji kukamilisha fomu zao kwa usahihi na mara wanapowasilisha hawataweza kurekebisha taarifa hizo iwapo huwakujaza kwa ufasaha.
Pia iliwataka waombaji kutunza nakala za maombi ya mkopo waliyowasilisha HESLB kwa matumizi mengine endapo itahitajika, pamoja na kuzingatia muda wa kutuma maombi.
Aprili 17, HESLB ilitangaza kuanza kupokea maombi kwa mwaka wa masomo 2018/19 kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi huu.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na bodi hiyo, mikopo hiyo ilikuwa ikisubiri maboresho ya mfumo wa uombaji mikopo kwa njia ya mtandao.
Katika taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao wa www.olas.heslb.go.tz.
Katika taarifa hiyo, Badru alisema kwa uzoefu wa miaka iliyopita waombaji wa mikopo waliwasilisha maombi yao bila kuzingatia mwongozo uliotolewa na kusababisha baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo.
"Mwaka jana (2017), kwa mfano, zaidi ya waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi ya 61,000 hawakuambatanisha nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au hata vile vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kama tulivyoelekeza," alisema.
Alitaja nyaraka nyingine muhimu ambazo waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni pamoja na nakala za vyeti vya kitaaluma za kidato cha nne, sita na stashahada ambazo zimethibitishwa na Kamishna wa Viapo - yaani wakili au hakimu.
Aidha, Badru alisema wanafunzi waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Kituo cha Afya cha Serikali.
Pia alisema wanafunzi ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya sekondari au stashahada (diploma) wawe na barua za uthibitisho wa udhamini huo kutoka katika taasisi zilizogharamia masomo yao
0 Comments